Katika siku ya pili ya Jukwaa hilo siku ya Jumatatu, Karen Hallberg, Katibu Mkuu wa Mikutano ya Pugwash kuhusu Sayansi na Masuala ya Dunia, amesema kuwa katika Asia ya Magharibi, “isipokuwa Israel, nchi zote ni wanachama wa Mkataba wa Kuzuia Uenezaji wa Silaha za Nyuklia (NPT), jambo linalodhihirisha dhamira yao ya pamoja ya kuzuia uenezaji wa silaha hizo.”
Hallberg ameongeza kuwa: “Zaidi ya hayo, kuna nia ya wazi miongoni mwa mataifa ya eneo hilo kutumia nishati ya nyuklia kwa njia za amani. Licha ya tofauti za kisiasa, kuna makubaliano ya pamoja kuhusu kutoueneza silaha za nyuklia.”
Amesema matumizi ya amani ya nishati ya nyuklia yanapaswa kuendelezwa katika mataifa yote, akiongeza kuwa “masharti ya Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA) yawe chombo cha kuthibitisha kuwa shughuli za nyuklia ni kwa madhumuni ya amani pekee.”
Paolo Cotta-Ramusino, Katibu Mkuu wa zamani wa Pugwash, pia amesisitiza tofauti ya msingi kati ya matumizi ya amani ya nishati ya nyuklia na silaha za nyuklia, akisema, “Maendeleo ya nishati ya nyuklia hayaonyeshi kwa lazima nia ya kutengeneza silaha za nyuklia. Matumizi ya amani ni muhimu sana kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi.”
Pugwash ni taasisi ya kimataifa inayojihusisha na kupunguza hatari zinazotokana na silaha za nyuklia na silaha nyingine za maangamizi makubwa. Kupitia mijadala isiyo rasmi baina ya wanasayansi, watunga sera, na wataalamu, taasisi hiyo hutoa suluhisho la kisayansi linalotegemea ushahidi kwa changamoto za usalama duniani.
Nasser Hadian, mhadhiri wa sayansi ya siasa katika Chuo Kikuu cha Tehran, amezngumza katika kikao hicho na kusema, “Israel ndio utawala pekee unaomiliki silaha za nyuklia katika eneo hili na hauoni sababu ya kuzitupilia mbali kwa sababu ya kile unachokiita usalama unaopata kutokana na silaha hizo.”
Rais Masoud Pezeshkian wa Iran katika ufunguzi wa Jukwaa la Mazungumzo la Tehran (TDF)
Jumapili, Rais Masoud Pezeshkian wa Iran alisisitiza kuwa, kama mwanachama wa Mkataba wa Kuzuia Uenezaji wa Silaha za Nyuklia (NPT), Iran ina haki ya kutumia teknolojia ya nyuklia kwa madhumuni ya amani na kufanya utafiti wa nyuklia kwa matumizi mbalimbali, yakiwemo ya afya, kilimo, viwanda na sekta nyingine muhimu.
Alisema imani za kidini za Iran haziruhusu utengenezaji wa silaha za nyuklia—silaha zinazoweza “kuangamiza ubinadamu na ambazo hazina cha maana cha kuchangia katika mustakabali wa dunia zaidi ya unyama.”
Iran imesema kuwa Israel ndicho kizuizi pekee cha kufanikisha eneo huru lisilo na silaha za nyuklia katika Asia ya Magharibi.
Israel inaendeleza sera ya ukimya wa makusudi kuhusu silaha zake za nyuklia na inakadiriwa kuwa na silaha za nyuklia kati ya 200 hadi 400, na hivyo kuifanya kuwa eneo pekee katika Asia ya Magharibi linalomiliki silaha hizo zisizo za kawaida.
Your Comment